Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Vincent Mashinji
amefunguka na kudai anajisikia uzito kuelezea hali ya Mbunge wa Singida
Mashariki Tundu Lissu inavyoendelea huku akimtaka aliyefanya kitendo
hicho ajitafakari.
Mashinji
ametoa kauli hiyo leo asubuhi wakati CHADEMA ikitoa msimamo wake na
kuelezea hali ya Mbunge huyo wa Singida Mashariki ambaye bado anapatiwa
matibabu nchini Kenya kufuatia kushambuliwa kwa risasi kwa mbunge huyo.
"Bado najisikia uzito wa
kuelezea jamii ya Watanzania hali ya kiongozi wetu Tundu Lissu, najua
nina jukumu kubwa kama mtendaji wa chama kutaarifu umma juu ya hali ya
Lissu inavyoendelea. Ni majonzi makubwa sana na kama kuna mtu katika
taifa hili alifanya hicho kitendo anatakiwa ajitafakari sana. Mpaka jana
asubuhi ameenza kupatwa na matatizo ya kifua kutokana na kulala
kitandani muda mrefu, na kwa sababu mguu wake wa kulia umevunjwa vunjwa
kwa risasi, nyonga yake pia mkono wake umevunjwa kwa risasi lakini
'inshallah' kama nilivyosema awali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayeamua
kuchukua roho ya nani na aache ya nani", amesema Mashinji.
Aidha, Mashinji
amesema wamemuumiza sana Lissu ila hawataacha kumpigania ili aweze
kupona na kutoka katika hali aliyokuwa nayo kwa sasa ili aweze kurudi
kuendelea kuwapigania Watanzania.
"Waswahili wanasema hujafa
hujaumbika, kwa kweli wamemuumiza kwa hiyo ndugu zangu hiyo hali ya
Lissu jana ilikuwa mbaya mpaka wakamuwekea mipira ya kupumulia lakini
ilipofika wakati wa mchana hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.
Tunasafari ndefu ya kuhakikisha Lissu anapona, sasa hivi wamemtibu zile
sehemu za ndani ambazo zingeweza kuhatarisha maisha yake kwa zile risasi
zilizopita tumboni na sehemu nyingine", amesema Mashinji.
Pamoja na hayo, Mashinji ameendelea kwa kusema "Mhe.
Lissu ni kweli tuliambiwa alipigwa risasi tano katika mwili wake lakini
kulingana na hali ya mwili ulivyobomolewa yawezekana zilizidi. Leo ni
siku ya tano akiwa anatibiwa hospitali na mpaka sasa hivi ameshafanyiwa
oparesheni tatu nadhani itabidi kuzisitisha kidogo ili kumpa ahueni
aweze kupumzika na yeye. Tulitegemea ingekuwa suala la kawaida tu yeye
kwenda kutibiwa na kurudi lakini imekuwa tofauti. Msilie wala kusononeka
kwa sababu Lissu bado yupo hai anaendelea kupigana na sisi, kuhakikisha
kwamba anapona na kurudi kuendeleza ukombozi Watanzania ili kufikia
uhuru wa kweli na mabadiliko ya kweli", amesisitiza Mashinji.
Kwa upande mwingine, Mashinji
amesema wanajiandaa kisaikolojia kumpokea Lissu na hali ambayo atarudi
nayo kwa kuwa hiyo ndiyo zawadi waliyopewa na Mwenyezi Mungu.
Comments
Post a Comment