Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuchangia damu
katika hospitali zote nchini kwa ajili ya kuienzi damu ya Mwanasheria
Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu iliyomwagika ,kwa kupigwa risasi na
watu wasiojulikana.
Akizungumza
na wanahabari leo katika makao makuu ya chama hicho, Katibu Mkuu wa
CHADEMA Taifa, Vicent Mashinji amewaomba wafuasi wa chama hicho waliopo
nchini Tanzania kuhakikisha kuanzia leo wanaenda kujitolea damu ili
kuwasaidi wagonjwa wenye uhitaji wa damu.
Dkt. Mashinji amesema kuwa, kutokana na
damu ya Lissu kumwagika kabla ya wakati wake ni vyema wanachama nao
wakaungana na kwa pamoja kutoa msaada huo ikiwa kama ishara ya
kulikomboa taifa la Tanzania.
"Damu ya Lissu imemwagika
nyingi sana, lakini watu waliofanya tukio hilo hawajatutisha bali
wametuimarisha. Lissu amemwaga damu yake kabla ya muda, Makamanda wote
twendeni hospitali zote nchi nzima kuchangia wagonjwa damu. Damu
tutakazochangia ni ishara ya kulikomboa taifa letu" Dkt. Mashinji
Ameongeza kwamba "Nategemea
kuanzia leo nitaanza kupata taarifa kutoka mahali mbalimbali nchini
Tanzania mkijitolea damu ili kuisaidia benki zetu za damu na wagonjwa
wote wakapate huduma ya damu kwa urahisi.
Aidha Mashinji amefafanua kuwa Lissu
kupelekwa Jijini Nairobi siyo kwamba hawawamini madaktari wa nyumbani,
bali wamehitaji kiongozi huyo aweze kupona haraka akiwa katika mazingira
yaliyotulia na yatakayomfanya apumzike kwa amani bila kuweweseka
kutokana na tukio lililomtokea
Pamoja na hayo Dkt. Mashinji ameweka
wazi kwamba matibabu ya kiongozi huyo yatagharamiwa na chama kwa kuwa
hawajafuata utaratibu wa bunge unavyohitaji.
"Suala la matibabu ya Mh.
Lissu Chama tutagharamia na hatuna wasiwasi katika hilo. Wanachama
pamoja na marafiki zetu wapo pamoja nasi na tumeshaanza kupokea michango
lakini kama kuna watu wanahitaji kutuchangia kufanikisha matibabu ya
Tundu Lissu watu wanaweza kutumia Akaunti Inaitwa CHADEMA M4C Bank
ya CRDB tawi la Mbezi 01J0180100600 Tuwashukuru wote na salamu za pole tumezipokea" Dkt. Mashinji.
Comments
Post a Comment