Translate

Juhudi Zinahitajika Ili kuongeza Ushiriki Katika Michuano ya kimataifa.

SERIKALI imeendelea kuvisisitiza vyama vya michezo kuhakikisha vinafanya kazi zao kwa mipango ya kuendeleza michezo husika ili kuiwezesha nchi ya Tanzania kupata washiriki wengi zaidi kwenye mcihuano ya kimataifa.
Waziri wa habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnaye alisema kwa sasa Tanzania imekuwa ikipeleka washiriki wachache kwenye mashindano ya kimataifa na kusababisha kukosa medali za aina yoyote ile.
Alisema Serikali ya awamu ya tano inadhamira ya kuona michezo mbalimbali inapiga hatua hapa nchini kama ilivyo kwa mataifa mengine duniani tofauti na sasa ambapo mpira wa miguu ukiwa maarufu zaidi.
Aliongeza kuwa katika kuhakikisha michezo inapiga hatua kubwa hapa nchini waliviagiza vyama vyote vya michezo kuandaa mpango kazi na kukabidhiwa kwa Baraza la Michezo Tanzania(BMT) ili wajue ni namna gani ya kutoa msaada.
Nape alidai licha ya kutoa agizo hilo, bado vyama mbalimbali vimeendelea kukaidi agizo lao jambo linalopelekea Serikali kutokujua mahitaji sahihi yanayohitajika katika vyama vya michezo pamoja na kuwapa ugumu wa namna ya utoaji wa misaada.
"Kiukweli hakuna mchezo wala kitu chochote kitakachokuwa na maendeleo kama hakutakuwa na mpango kaz na hivyi vyama vya michezo tumeviagiza makusudi vilete mipango kazi yao lakini mpaka sasa utekelezaji wake umekuwa ni wa kusuasua," alisema Nape.
Pia Nape alisema Serikali haitosita kuvichukulia hatua kali na za kinidhamu vyama vyote vya michezo vitakavyoendelea kukiuka agizo hilo hilo walilolitoa ili kujenga uwajibikaji wa kutosha katika sekta ya michezo.
Wakati huo huo, Nape ameitaka Kamati ya Mashindano ya Olympiki pamoja na BMT kuhakikisha wanahamasisha washiriki wengi kutoka michezo mbalimbali hapa nchini wanakwenda kushiriki mashindano ya Olympiki 2020 yatakayofanyika Tokyo, Japan.
Alidai endapo kutakuwa na idadi kubwa ya washiriki kutaiweka Tanzania katika sehemu nzuri ya kutwaa tuzo nyingi tofauti na sasa ambapo washiriki wamekuwa wachache na idadi ya tuzo zinazochukuliwa katika mashindano hayo imekuwa ni duni na kutoridhisha.
"Mimi ndio kiongozi wa hii Wizara inayohusika na michezo, ningependa kuona katika mashindano yajayo ya Olympiki tunarudi na tuzo za kutosha kama vile mataifa mengine ulimwenguni yanavyofanya na pia naona uwezo wa kutwaa tuzo hizo tunao," aliongeza Nape.


Follow Us:
https://www.facebook.com/msechuJRhttps://www.instagram.com/officialhumphreymsechu/https://twitter.com/msechuhumphreymsechuhumphrey@gmail.com




Comments