Translate

Taarifa kutoka TFF yausikitisha uongozi wa klabu ya majimaji.


HATIMAYE Uongozi wa klabu ya Majimaji FC umeonesha kusikitishwa na maamuzi yaliyotolewa na kamati ya masaa 72 kwa ushirikiano na bodi ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kudai kuwa maamuzi hayo yametolewa kiupendeleo.

Uongozi huo umelalamikia maamuzi ya kamati kutokana na mapungufu yaliyojitokeza wakati wa mchezo kati yao na Yanga uliopigwa uwanja wa Majimaji Mjini Songea, Mkoani Ruvuma juma lililopita na Klabu ya Majimaji kuchezea kichapo cha bao 1-0.

Kamati ya saa 72 ilitangaza kumfungia mwamuzi aliyechezesha mchezo huo, Hussein Athuman kwa madai ya kupata alama za chini ambazo hazimwezeshi kuendelea tena kuchezesha Ligi hiyo.

Pia Kamati hiyo iliipiga faini klabu ya Yanga kwa makosa ya kuvunja kanuni za ligi kuu Tanzania bara (VPL) baada ya kukaidi kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia pamoja na kutumia mlango ambao haukustahili wakati wakiingia uwanjani hapo.


Afisa habari wa Majimaji FC, Nathan Mpeja alisema kitendo cha mwamuzi kufungiwa kinadhihirisha ni jinsi gani mechi hiyo ilivyokuwa na madudu mengi na kuendelea kuacha matokeo yawepo kama yalivyo yanaibeba klabu moja na kudai kuwa kitendo hicho hakiwezi kuinua soka la Tanzania.

"Sasa sisi tunajiuliza kama mwamuzi aliendesha vibaya ile mechi yetu tuliyocheza wiki iliyopita na wameshatangaza kumfungia kwa kile wanachodai hana uwezo wa kuendelea kufundisha, sasa kwa nini hawabadilishi matokeo pia ambayo yalipatikana katika mchezo huo uliochezeshwa chini ya kiwango?," alisema Mpeja
.

Wakati huo huo uongozi wa Majimaji FC umeiandikia barua bodi ya Ligi wakiitaka kusogeza mbele mchezo wao wa ligi kuu ya soka Tanzania bara utakaochezwa mwishoni mwa juma hili dhidi ya Ndanda FC mjini Mtwara.

Akizungumzia juu ya ombi lao hilo, Mpeja alisema wameamua kuandika barua hiyo ya kuomba mchezo wao kusogezwa mbele kutokana na kuwepo kwa baadhi ya sababu muhimu zilizo nje ya uwezo wao.

"Kwa sasa nisingependa kusema zaidi kuhusu sababu tulizoziandika lakini naomba watanzania na wapenzi wa Majimaji kwa ujumla watambue kwamba tumeomba mchezo wetu upelekwe mbele kidogo," alidai Mpeja.

Comments