SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania limewataka mashabiki wa soka nchini kuwa na Subra kuhusu hatima ushiriki waTimu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, (Serengeti Boys) katika fainali za mataifa Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17.
Timu ya Serengeti Boys ilikata rufaa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika(CAF) mara baada ya kufungashiwa virago na timu ya Congo Brazaville katika mashindano ya kutafuta tiketi ya kufuzu kucheza mashindano hayo huku madai makubwa yakielezwa Congo Brazaville kumtumia mchezaji Langa Leccy Bercy aliyezidi umri katika michezo yao yote miwili.
Afisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema bado wanaendelea kusikilizia hatma ya suala hilo mara baada ya siku 10 walizozitoa CAF kwa Congo Brazaville kumalizika tangu jumapili huku mchezaji huyo akishindwa kupelekwa mbele ya wataalamu kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya umri.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za awali walizozipata kutoka kitengo cha habari na mawasiliano cha CAF zimeeleza kamati tendaji ya shirikisho hilo itatoa maamuzi ya suala hilo mara baada ya kukamilika kwa mashauriano ambayo watayafanya.
"Niwatake watanzania kuondoa wasiwasi juu ya suala hili la Langa Bercy kwa sababu sisi tulishatimiza yale tuliyokuwa tunatakiwa kuyafanya, na wao Congo Brazaville walitakiwa wafanye walichoagizwa na badala yake wameshindwa kutekeleza maagizo waliyopewa kwa hiyo ngoja tuangalie maamuzi yatakayochukuliwa na CAF," alidai Lucas.
Katika hatua nyingine Lucas aliongeza kuwa fainali za mataifa Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 zilizotakiwa kufanyika nchini Madagascar hazitofanyika huko na badala yake zitafanyika nchini Congo Brazaville.
Alieleza kuwa wamepewa taarifa kutoka CAF kwamba michuano hiyo itafanyika nchini Congo Brazaville mara baada ya shirikisho hilo kubaini baadhi ya mapungufu kwa nchi ya Madagascar ambao walitangazwa kuwa ndio waandaaji wa fainali hizo.
"Nadhani wengi wanatambua kwamba fainali hizi za vijana walio chini ya miaka 17 zilitarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi wa pili huko nchini Madagascar kwa hiyo kutokana na mabadiliko haya yaliyotangazwa na CAF mashindano hayo yatafanyika tarehe ileile iliyopangwa huko nchini Congo Brazaville," alieleza Lucas.
Follow Us:




Comments
Post a Comment