RAIS John Magufuli alisema serikali iko tayari kufanya mchakato wa kurekebisha sheria na kuzifikisha bungeni ili Katiba mpya iweze kupatikana. Alisema sehemu ilikofikia mchakato huo ni pazuri ndio maana serikali yake itayashughulikia mambo ambayo inatakiwa kuyafanya ili Kura ya Maoni ya Katiba ifanyike.
Rais Magufuli aliyasema hayo Ikulu, Dar es Salaam jana baada ya kupokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana aliyokabidhiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) chini ya Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Damian Lubuva.
Alimpongeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa kufikisha mchakato wa Katiba sehemu hiyo. “Kwa kweli Mheshimiwa Kikwete umenipunguzia kazi katika suala hili la Katiba, mimi naahidi kuanzia pale ulipoishia wewe,” alisema Rais Magufuli akimueleza Kikwete, ambaye alikuwa mmoja wa waliohudhuria hafla hiyo.
Awali, NEC ilisema kuwa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa haijakwama na Rais Magufuli aliridhia mchakato huo kuendelea mara baada ya sheria ya kura hiyo ambayo imepitwa na wakati kurekebishwa na Bunge.
Jaji Lubuva alisema kuwa mchakato huo haukuwahi kukwama bali uliahirishwa kutokana na tume hiyo kushindwa kuhimili mzigo wa kuendesha uchaguzi mkuu na kura ya maoni kwa pamoja.
“Aprili 2, mwaka jana tulitangaza kuahirishwa kwa kura ya maoni, hii ni baada ya Rais kuikabidhi tume Katiba inayopendekezwa kuelekea kura ya maoni kufanyika Aprili 30, sababu za kuahirisha ni kutokana na uandikishaji wa wapiga kura kutokukamilika,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema tume isingeweza kuendesha na kusimamia jambo zito kama kura ya maoni sambamba na Uchaguzi Mkuu kwa wakati mmoja. Alisema kwa kuwa Uchaguzi Mkuu umemalizika, sasa tume inajielekeza katika majukumu mengine yanayohusu kazi za tume likiwemo la kura ya maoni.
Alisema kwanza wataangalia sheria ya kura ya maoni namba 11 ya mwaka 2013 ambayo alikiri kuwa maeneo mengi yamepitwa na wakati. Aliongeza kuwa NEC na ZEC wataangalia kwa pamoja maeneo mbalimbali ya sheria hiyo kwa lengo la kuifanyia marekebisho sheria ya kura ya maoni.
“Mapendekezo ya marekebisho yatafikishwa serikalini na kwa utaratibu wa kawaida, itaandaa mswada wa marekebisho ambao utafikishwa bungeni,” alisema Jaji Lubuva na kuongeza kuwa baada ya hapo tume hiyo itaendelea na mchakato wa kura ya maoni mara itakapotengewa fedha na Serikali.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amehakikisha Rais mstaafu Kikwete kuwa yuko salama, licha ya kuwa kuna watu wanasema maneno aliyoita ya ovyo ovyo kuwa ashitakiwe kwa kukwamisha mchakato wa Katiba.
“Watachonga, lakini yakizungumzwa yaweke pembeni, wastaafu wote kuweni na amani na mimi ndio kazi yangu kuwalinda ili msije mkajiona kuwa mkistaafu ndio mwanzo wa kunyanyasika,” alisema Rais Magufuli.
Hivi karibuni mwanahabari nguli Jenerali Ulimwengu alipendekeza Kikwete ashitakiwe, kwa maelezo kuwa aliidhinisha kutumika kwa mabilioni ya fedha za walipa kodi katika mchakato wa Katiba wakati umekwama.
Akizungumzia siasa, Rais Magufuli amewajibu wanasiasa wanaodai kunyimwa haki ya kikatiba ya kufanya mikutano kwamba uchaguzi umeisha na sasa ni wakati wa serikali iliyochaguliwa kutekeleza ahadi ilizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni.
Rais Magufuli alisema haiwezekani kila siku watu kufanya siasa, na kwamba serikali iliyopo madarakani ni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na yeye kama Rais kuna mambo aliyowaahidi wananchi kuyashughulikia ili kutatua kero zao, hivyo hayuko tayari kuona mtu yeyote anamchelewesha kutekeleza ahadi hizo ndani ya miaka mitano.
“Kuna mambo tuliahidi kwa wananchi, nisingependa kuona mtu yeyote ananichelewesha kuyatekeleza hayo niliyoahidi...katika kipindi cha miaka mitano, niwaombe wanasiasa wenzangu ushindani wa sasa hivi wa vyama vya siasa unatakiwa uweke nguvu zaidi kwa wale wawakilishi waliopewa mamlaka na wananchi,” alisema Magufuli.
Alisema ushindani wa siasa ubaki kwa viongozi ambao wamepewa ridhaa na wananchi wakati wa uchaguzi “kama ni diwani wapeleke hoja za nguvu katika eneo lake la kata na kama ni mbunge akazungumze kwa nguvu bungeni na katika eneo lake, hiyo ndio demokrasia.”
Aliahidi kusimamia msimamo wake huo kwa nguvu zote kwamba uchaguzi umeisha na sasa ni wakati wa kufanya kazi na kutoa fursa kwa serikali iliyopo madarakani kusimamia na kuelekeza ahadi ilizozitoa.
“Hata katika nchi zilizoendelea, huwezi kukuta kila siku ni siasa, ni siasa, ni vyema tutimize wajibu wetu tuliopewa na wananchi, mimi niko tayari kushirikiana na wanasiasa wenzangu kushughulikia changamoto zinazotukabili kama taifa, ili nchi yetu iweze kusonga mbele,” alisema Rais Magufuli.
Alitoa mwito kwa wanasiasa wenzake kumwelewa kwamba lengo lake ni kutaka kushughulikia matatizo ya Watanzania na akaongeza kuwa Watanzania wanataka maendeleo na kero zao ziondolewe na sio kila siku watu kufanya siasa.
Alisema kwa mtazamo wake baada ya uchaguzi kumalizika, hakuna Mtanzania aliyeshinda wala aliyeshindwa, bali wote ni washindi na sasa wote wanatakiwa kufanya kazi. Akizungumzia taarifa ya uchaguzi wa mwaka 2015, Rais Magufuli amekiri kuwa uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkali na mvuto ndani na nje ya nchi.
Alisema baadhi ya watu waliamini kuwa kutokana na ushindani ule kungetokea vurugu mara baada na wakati wa uchaguzi. Aliwashukuru viongozi wa vyama vya siasa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha kwamba mchakato wa uchaguzi ulimalizika salama bila kuwepo vurugu yoyote.
Aliipongeza tume ya uchaguzi kwa maelezo kuwa kama isingesimamia uchaguzi vizuri, kungeweza kutokea vurugu kama ilivyowahi kutokea katika nchi zingine. Alisema kasoro zilizojitokeza na kusababisha kukosolewa na baadhi ya wanasiasa, tume hiyo izifanyie kazi ili uchaguzi ujao uwe bora zaidi.
Magufuli alitoa kauli hiyo wakati kukiwa na malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa vya upinzani kuwa kiongozi huyo anaminya demokrasia kwa kutowaruhusu kufanya mikutano ya siasa kama katiba inavyoelekeza.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hivi karibuni kilifungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kupinga uamuzi huo wa serikali, hata hivyo, kesi hiyo ilitupiliwa mbali na mahakama kutokana na walalamikaji kutotimiza vigezo vya kisheria.
Rais Magufuli pia alitumia fursa hiyo kuzungumzia suala la Zanzibar kwamba hakuingilia mgogoro wa uchaguzi kisiwani humo kwa sababu katiba haimruhusu kufanya hivyo. “Wale waliokosoa ZEC (Tume ya Uchaguzi Zanzibar) ndio waliokuja kwangu wakitaka niingilie masuala ya Zanzibar, mimi nilikataa kwa sababu naheshimu katiba,” alisema Magufuli.
Alisema alichoahidi ni kwamba amani inadumishwa Zanzibar wakati wote wa mchakato wa uchaguzi na hilo akaeleza kuwa alilitimiza kwani wananchi wa Zanzibar walifanya uchaguzi wa marudio kwa amani.
“Nawapongeza ZEC kwa kusimamia uchaguzi vizuri, tena nyinyi mlifanyau chaguzi mbili kwa kweli nawapongeza sana...nampongeza Jecha (Salum Jecha ambaye ni mwenyekiti wa ZEC) kwa kusimamia uchaguzi ule kwa weledi mkubwa,” alisema Magufuli.
Wakati huo huo, utafiti uliofanywa na Taasisi Huru ya Kijamii ya CZI katika mikoa 15 nchini kuhusu utendaji kazi wa Rais John Magufuli, umebaini kuwa rais anakubalika kwa wananchi kwa asilimia 89 tangu aingie madarakani.
Hayo yamo kwenye taarifa ya matokeo ya utafiti uliofanywa Tanzania Bara na Visiwani, kuangalia utendaji kazi wa rais kwa miezi minane tangu aingie madarakani; anaripoti Ikunda Eric.
Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, jopo la watafiti hao likiongozwa na mwanadiplomasia kijana Dotto Nyirenda, walisema walihoji makundi matatu ya watu.
Nyirenda alisema kwa ujumla rais anakubalika kwenye jamii kwa asilimia 89 na hiyo inatokana na majibu ya utafiti huo kutoka makundi matatu yaliyohojiwa. Kundi la kwanza lililohojiwa ni vijana wenye umri wa miaka 14 hadi 18 ambalo lilisema wanaamini Rais Magufuli ataleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kurejesha nidhamu ya masomo shuleni.
Nyirenda alisema kundi hilo linaamini kwa asilimia 78 utendaji kazi wa Rais Magufuli na kwamba ataleta mageuzi kwenye elimu, ikiwa ni pamoja na kuondoa tatizo la madawati, mitaala na kurudisha nidhamu ya walimu.
Hata hivyo, katika kundi hilo asilimia 22 wanaona huenda rais asifanikiwe kwenye sekta ya elimu na pia kuondolewa kwa michezo shuleni kutadidimiza maendeleo ya michezo nchini.
Kundi la pili lililohojiwa ni vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 30 wanaoamini utendaji kazi wa rais kwa asilimia 82, na kwamba ataleta mabadiliko kwenye sekta ya ajira na elimu kwa sababu amelivalia njuga tatizo la watumishi hewa na ajira za kwa wahitimu zitapatikana kwa kiasi fulani tofauti na ilivyokuwepo tatizo la watumishi hewa.
Kundi la tatu ni wananchi wenye umri wa miaka 30 hadi 60 ambao asilimia 89 walisema upo uwezekano wa watumishi wa umma kurejesha imani kwa serikali kutokana na juhudi za rais alivyopambana na ufisadi na rushwa.
Pia kundi hilo linaamini kwa rais atamaliza matatizo ya wazee kwa kuanza kuwalipa posho kwa mwezi lakini pia wanaamini nidhamu ya watumishi wa umma itaongezeka. Mikoa iliyofanyiwa utafiti ni Tanga, Dodoma, Kusini Pemba, Kaskazini Unguja, Tabora, Kigoma, Simiyu, Morogoro, Pwani, Arusha, Manyara, Geita, Mara na Ruvuma.

Comments
Post a Comment