RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein ameongoza mamia ya wananchi katika kisomo cha ibada ya hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amaan Karume aliyetimiza miaka 44 tangu alipouawa Aprili 7, 1972.
Kisomo cha ibada ya hitma kilianza kwa dua iliyosomwa na Mufti Mkuu wa Tanzania, Alhaji Shehe Abubakar Zubeir na baadaye kusomwa Kuran tukufu na Shehe Sharif Abdulrahman ikiwa ishara ya kuanza shughuli hiyo kwenye Makao Makuu ya CCM Kisiwandui mjini Unguja.
Akitoa mawaidha katika ibada ya hitma, Mjumbe kutoka katika Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) Shehe Hamid Masoud Jongo alisema kipimo cha mtu bora mbele ya Mwenyezi Mungu, ni yule aliyefanya mambo makubwa kwa maslahi ya wananchi walio wengi ikiwa ni kauli ya Mtume Muhammad (SAW).
Jongo alisema kazi kubwa iliyofanywa na hayati Karume ikiwemo kuleta umoja na mshikamano pamoja na kuongoza Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 na kuwaunganisha wananchi wa pande mbili hizi kwa kuwepo kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni sehemu ya matunda ambayo wananchi wanafaidika nayo hadi leo.
Kwa mfano, alisema Muungano umewanufaisha wananchi wengi kwani wapo Wazanzibari wanaofanya shughuli zao za kibiashara na kujenga majengo makubwa Tanzania Bara bila ya bughudha sambamba na watu wa Tanzania Bara kuwapo Zanzibar wakifanya kazi zao bila ya usumbufu.
“Huyo ndiye kiongozi mwema ambaye hapa katika kipindi kifupi tulikuwa tukimuombea dua kutokana na mchango wake wa kufanya kazi kwa maslahi ya wananchi wenzake katika kufanya mambo mema kwa maslahi ya wengi,” alisema Shehe Jongo ambaye ni Imamu wa Msikiti wa Manyema jijini Dar es Salaam.
Mapema, Dk Shein aliongoza kazi ya kuweka shada la maua katika kaburi la marehemu Karume na kufuatiwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alimwakilisha Rais John Magufuli aliye safarini Rwanda.
Aidha, Balozi Ali Karume pamoja na mjukuu wa hayati Karume, Ahmed Amani Abeid Karume waliweka mashada ya maua kwa niaba ya familia ya marehemu huku Rais mstaafu Amani Abeid Karume akishuhudia.
Shughuli hiyo ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa kitaifa ambao ni Makamu wa Rais Samia, mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein pamoja na mjane wa marehemu, Fatma Karume.
Aidha, ibada hiyo ilihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano Ali Hassan Mwinyi pamoja na Makamu wa Rais mstaafu wa Muungano, Dk Mohamed Gharib Bilal.
Wengine waliojumuika ni wanafamilia na watoto wa marehemu akiwemo Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume na Balozi Ali Karume ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na mtoto wa pili wa marehemu.
Karume aliuawa kikatili na wapinga maendeleo Aprili 7, 1972 katika yaliyokuwa Makao Makuu ya chama cha ASP Kisiwandui mjini hapa wakati akiwa na viongozi wenzake wa chama wakicheza mchezo wa dhumna.
Hayati Karume kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa ASP ndiyo waliofanikisha Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ambayo yaliung’oa utawala wa kisultani na wananchi wazalendo kushika hatamu ya kuongoza Dola.
Hadi anauawa, Karume alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mwenyekiti wa Afro Shiraz Party (ASP) na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano chini ya Mwalimu Julius Nyerere

Comments
Post a Comment