Meneja wa viongozi wa ligi hiyo Leicester City Claudio Ranieri alibubujikwa na machozi baada ya kufurahishwa na vijana wake walipoitandika Sunderland kwa mabao 2-0.
Ushindi huo uliongeza uwezekano wa timu hiyo kutawazwa mabingwa wa Premier League kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo, baada ya kufungua mwanya wa pointi 7. Alikuwa Jamie Vardy aliyeipa ushindi Leicester kwa kupachika mabao mawili muhimu juzi Jumapili.
Na Tottenham Hotspurs iliyoko katika nafasi ya pili ilipachika mabao matatu dhidi ya Manchester United juzi Jumapili, kipigo ambacho kina maana Leicester imejihakikishia kuwamo katika timu nne za juu ambazo zitashiriki katika michezo ya Champions League msimu ujao.
Kocha wa Manchester United Louis van Gaal amesema kwamba hajutii kutochukua kazi ya kuifunza Tottenham Hotspurs baada ya timu hiyo ya mjini London kuchafua matumaini ya timu yake kucheza katika Champions League juzi.
Arsenal nayo imepoteza mwelekeo baada ya kulazimisha sare ya mabao 3-3 dhidi ya West Ham United siku ya Jumamosi.
Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp anaamini kijana chipukizi Divock Origi yumo mwanzoni mwa kitu muhimu baada ya kupachika mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Stoke City juzi Jumapili. Klopp anahisi Origi ataimarika siku hadi siku, akisema yuko katika njia nzuri , na hii ni msingi mzuri na sasa watafanyakazi kwa pamoja kufikia lengo lake.

Comments
Post a Comment