Translate

Muhongo: Asilimia 89 bajeti ya kwenda kwenye maendeleo

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema bajeti ya wizara hiyo asilimia 89.5 ni ya maendeleo, hivyo matumizi ya kawaida yatapunguzwa na mengine kama vile ‘bonus’ kwa mashirika na taasisi za wizara hiyo yamefutwa.

Profesa Muhongo alisema hayo jana wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo lililoshirikisha wawakilishi wa taasisi na mashirika yaliyo chini ya wizara hiyo.
Alisema bajeti hiyo imejikita katika maendeleo huku matumizi ya kawaida yakipungua na kuwataka wafanyakazi kujitathmini na kujinyima kwani hata fedha kidogo za matumizi zinatakiwa kupelekwa katika sehemu za kukusanya mapato na kuwataka kujadili vipaumbele.
Profesa Muhongo alisema katika bajeti ya umeme vijijini, awali ilikuwa na Sh bilioni 300, lakini sasa wameongeza kwa asilimia 49.6 na kuwa karibu Sh bilioni 500 hivyo ni muhimu katika kikao hicho, wajadili utendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Akizungumzia kusitishwa kwa ‘bonus’ kwa taasisi na mashirika ya umma yaliyo chini ya wizara hiyo, Muhongo alisema matumizi hayo yamesimamishwa mpaka watakapokaa vizuri.
“Hili azimio mpitishe hivi, msione aibu na ujumbe ufike kwenye mashirika na taasisi za umma kwamba kuanzia sasa bonus hakuna na fedha nyingi tunapeleka kwenye shughuli za maendeleo,” alisema.
Profesa Muhongo alisema anajua Tanesco watamchukia, kwa kuwa walikuwa wakijigawia bonus ya kati ya Sh milioni moja hadi Sh milioni 50 kwa mtu mmoja, lakini yeye ataendelea kufanya kazi yake kwa manufaa ya Watanzania.
Alisema anaishangaa Tanesco kwa kugawana fedha hizo na kuhoji ni kwa manufaa ya kazi ipi wakati umeme unakatika hovyo ndio maana ameona fedha hizo zikafanye masuala maendeleo.
Waziri alitoa mfano wa nguzo ndogo za kusambazia umeme kuwa zimepungua wakati nguzo moja inauzwa Sh 300,000 na kuhoji kwa nini mtu mmoja ajilipe bonus ya zaidi ya Sh milioni 50 wakati kijijini kwao kuna Watanzania hawana nguzo.
Akijibu maombi ya wafanyakazi yaliyosomwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE), Marcelina Mushumbusi, kutaka kuwepo na bonanza, usafiri wa wafanyakazi, kuongezewa mabasi mawili na ufinyu wa nafasi za ofisi, Waziri Muhongo aliwaambia suala la bonus halina tofauti na bonanza ambavyo kwa sasa havitakuwepo.
Alisema yeye hatashiriki bonanza wala kwenda maeneo ya fukwe kula na kunywa na wafanyakazi kwani kwa sasa hakuna fedha hizo.
Kuhusu maombi ya kuongezewa mabasi mawili ya kubeba wafanyakazi yaliyotolewa na chama cha wafanyakazi, Muhongo alisema hawezi kuwaongezea basi na kuwataka waache mtazamo wa zamani bali waombe kuunganishwa na mabenki ili wapate mikopo na kununua mabasi yao.

Comments