WAFANYABIASHARA wanashauriwa kuzingatia maoni na mtizamo wa wengi kuhusu njia zinazotumika kukuza biashara
kuboresha bidhaa na huduma. Hata hivyo haulazimishwi kupuuza mbinu zako nzuri za kukuza biashara, ikiwa hazikatazwi kisheria.
Wataalamu wa biashara kutoka katika maeneo mbalimbali wanaochangia kwenye mtandao wa maswali, www.ask.com wanasema katika maelezo wanayoyatoa kwa nyakati tofauti kuwa, si wakati wote mtazamo wa wengi ni sahihi. Wanasema, mfanyabiashara anaweza kuwa na mtazamo wake mzuri na bora zaidi, ukihusisha mbinu mbalimbali za kuinua biashara yake,lakini akajikuta akikatishwa tamaa na maoni ya wengi kuhusu mbinu hizo na kujikuta akibadilika na kuanguka kibiashara.
Www.ask.com inaeleza kuwa, mfanyabiashara anawajibika kusikiliza mawazo ya wateja na wakati mwingine kufuatilia maoni ya wafanyabiashara wenzake kuhusu mambo tofauti ya kibiashara, lakini inawezekana mawazo hayo ya wengi yasimuinue kibiashara kama inavyotegemewa. Kwa maana hiyo, inaelezwa kuwa, mfanyabiashara anapaswa kuhakikisha anazingatia sheria katika uchaguzi wa mbinu hizo, kuhakikisha hakwazi wengine na kuona endapo zinaweza kumvusha kutoka katika ngazi moja ya kibiashara hadi kuifikia nyingine.
“Wapo wanaotoa maoni kwa nia ya kufanikisha na wengine wanafanya hivyo ili kuhakikisha mkakati wao wa kuibomoa biashara ya mtu au kikundi fulani unafanikiwa. Kwa sababu hiyo, ni lazima mfanyabiashara awe makini zaidi,” unaeleza mtandao wa www.ask.com. Mtandao huo unaeleza zaidi kuwa, msimamo kuhusu mbinu bora za biashara alionao mfanyabiashara, unategemea busara yake, elimu ya biashara aliyonayo pamoja na wakati husika.
Unasema kwa kuzingatia matakwa ya wateja katika soko, mfanyabiashara pia anakuwa na nafasi nzuri ya kupata mafanikio, zaidi ya kutegemea maoni ya watu fulani au kikundi fulani pekee, bila kufahamu kuwa wakati mwingine kati ya watoa mitazamo au mawazo hayo hakuna mnunuzi wa huduma au bidhaa anazoziuza. Inaelezwa kuwa, sababu ya kutoyatumia, ikiwa haitamkwaza mtoa mawazo inaweza kuelezwa bayana.
Kadhalika, mfanyabiashara ikiwa haitakuwa na umuhimu, anaweza kuachana na utaratibu wa kutoa sababu ya kwanini hakutumia maoni au ushauri wa mtu mwingine, kwa kuwa anayolazimika kuyatumia ni yale anayoamini kuwa yatamsaidia na si vinginevyo. Mbali na mtandao huo, mwingine wa majibu; Www.answers.com unasema kuwa, utaalamu kuhusu mbinu za biashara unaweza kutolewa na mfanyabiashara mwingine mwenye uzoefu kuhusu mbinu za biashara au mshauri aliyejifunza mbinu hizo.
Lakini, mtandao huo unaonya kuwa, licha ya kupokea maoni mengi kutoka kwa watu tofauti pamoja na ushauri kuhusu mbinu mbalimbali za biashara zilizo bora, mfanyabiashara anaweza asifanikiwe ikiwa hatafahamu anafanya biashara katika mazingira gani.
“Kwa maana hiyo, inapolazimu, mfanyabiashara anaweza kutoyatumia maoni ya watu kuhusu mbinu za kutumia katika biashara yake ili ajipe nafasi ya kuyasoma mazingira, zikiwemo mbinu zinazotumiwa na wenzake kufanya biashara,”www. answers.com inaeleza. Mtandao huo wa majibu unaongeza kuwa, hata akipewa maoni mazuri kiasi gani, ikiwa hatafahamu aina ya wateja au wahitaji wa bidhaa na huduma anazozalisha, licha ya kujua wakati gani azalishe nini, mfanyabiashara anayesikiliza maoni kuhuus mbinu za kiufundi hatafanikiwa.
Cha msingi kinachoelezwa katika www. answers.com ni mfanyabiashara kuwa makini kuangalia aina ya maoni au ushauri wa kuutumia, bila kujali umetolewa na idadi gani ya watu, kwa sababu si kila wakati ushauri wa wengi ni mzuri. Unaonya kuwa inaweza kutokea kuwa miongoni mwa watu 30 wanaoshauri itumike mbinu X ya biashara ili kuikuza, watano tu ndio wateja halisi wa biashara husika inayotolewa ushauri.
naelezwa kuwa, wakati mwingine maoni ya wengi huwa ni mwongozo mzuri hivyo hayapaswi kutupwa bila sababu za kitaalamu za msingi. Kubwa analolitaka mfanyabiashara ni kuyafikia malengo na mafanikio ya kibiashara kwa kukuza mtaji na ‘kulishika’ soko lililopo, pamoja na kuliongeza katika maeneo nje ya yaliyozoeleka. Kutokana na hilo, inaelezwa kuwa mfanyabiashara anapaswa kuangalia ushauri unaofaa na kuuchukua, huku akiupa kisogo usio faa.
Sambamba na hayo, mitandao hiyo miwili inasema kuwa, mfanyabiashara anatakiwa kutozingatia sura, umbo wala aina ya ukaribu alionao kwa mtoa maoni na mtazamo, bali aangalie ushauri unaotolewa kwakuwa si wakati wote pia asiyempenda anatoa usiofaa.
Kufuatia ukweli huo, mtndao huo unaeleza kuwa, anachotakiwa kukifanya mfanyabiashara husika ni kuhakikisha anakuwa makini wakati wote katika uchaguzi wa ushauri wa kuutekeleza.
Comments
Post a Comment