Translate

Bunge laita wadau kujadili sakata NSSF

Wajumbe wa kamati ya sheria wakiwa pamoja
Wajumbe wa kamati ya sheria
SAKATA la madai ya kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limeendelea kuchukua sura mpya baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuwaita wadau mbalimbali kujadili suala hilo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohammed Mchengerwa aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba walioitwa katika kikao hicho kitakachofanyika Aprili 25, mwaka huu mjini Dodoma ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na watendaji wa Wizara ya Kazi, Ajira, Sera na Watu wenye Ulemavu iliyochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Wengine ni viongozi wakuu wa Shirika la NSSF na wakaguzi wote wa ndani na nje ambao kwa njia moja au nyingine wamewahi kutumika katika ukaguzi wa miradi iliyo chini ya shirika hilo nyeti. Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumzia kukamilika kwa shughuli za kamati hiyo inayosimamia Wizara tatu za Katiba na Sheria, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Wizara ya Kazi, Ajira, Sera na Watu Wenye Ulemavu.
Kuhusu NSSF, alisema Kamati katika ufuatiliaji wake ilibaini kuwepo kwa taarifa nyingi zenye upungufu kuhusu uwekezaji na utendaji ndani ya NSSF, hivyo iliona vizuri kupata taarifa za CAG kuangalia ukaguzi wake katika shirika hilo. “Ili kujiridhisha tuliona ni vyema tukipata taarifa ya CAG. Lakini kama mnavyojua taarifa ya CAG hivi sasa ipo mikononi mwa Rais (John Magufuli) na kwa mujibu wa Sheria, ni lazima kwanza Rais awasilishe taarifa hiyo bungeni ndio sasa ianze kujadiliwa,” alisema mwenyekiti huyo na kuongeza:
“Kwa msingi huo, tumeona tusubiri kwanza Rais aiwasilishe bungeni taarifa ya CAG halafu kwa kanuni zetu za Bunge, taarifa ya NSSF itakuja kwetu ili tuichambue na ni wakati huo sasa tutamtaka CAG, viongozi wa Wizara na viongozi wa NSSF kufika mbele ya Kamati kutupa majibu kabla ya Wizara kuwasilisha bajeti yake bungeni.
“Lengo letu ni kutaka kujiridhisha kwanza, maana kama mnavyojua fedha zilizopo NSSF si fedha za umma, bali ni za wafanyakazi na wastaafu na kama mnavyojua mambo mengi yanasemwa kuhusu NSSF, hatua inayowafanya wachangiaji kuchanganyikiwa na wengi sasa hivi wanataka kujitoa.”
Alisema endapo kamati hiyo itapata taarifa za uhakika kupitia ripoti ya CAG itakayowasilishwa na Rais bungeni, lakini pia kupitia kikao hicho ilichokiitisha, itakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa maagizo wakati suala hilo litakapoanza kujadiliwa ndani ya Bunge na hivyo kukata kiu ya wananchi. Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo alisema Kamati hiyo imeiagiza Serikali na Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kufanya utafiti wa kina kuona kama Tanzania inahitaji kuendelea kuwa na lundo la mifuko ya hifadhi ya jamii inayofanya kazi zinazofanana.
“Tumewaagiza wafanye utafiti wa kina kuhusu jambo hili maana hivi sasa tuna karibu mifuko sita, inafanya kazi zinazofanana, watu ni wale wale, gharama za uendeshaji ni kubwa kwa vile yote ina wakurugenzi wanaolipwa fedha nyingi na stahiki mbalimbali. “Kwa nini tusiangalie uwezekano wa kuwa na mifuko miwili yaani wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi na mmoja ukashughulikia mambo kama ya kilimo na mwingine mambo ya afya,” alisema Mchengerwa.
Bajeti ya Katiba na Sheria Akizungumzia maagizo ya Kamati hiyo kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti huyo alisema msukumo mkubwa umekuwa juu ya kutengwa fedha kidogo kwa sekta ya sheria na hasa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), jambo linalotia shaka mustakabali wa utoaji wa haki.
Alisema wakati taifa likiwa katika mchakato wa kutengeneza Mahakama Maalumu ya Kushughulikia Ufisadi, fedha zinazotolewa kwa mishahara, nyumba na posho za Mawakili wa Serikali ni kidogo, hatua inayowafanya kufanya kazi katika mazingira magumu ukilinganisha na mawakili binafsi, suala ambalo ni la hatari.
Jengo la Makamu wa Rais Aidha, kamati hiyo imemuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kukagua ubora wa ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais, baada ya kuwepo wasiwasi wa ubora wake.
Pia imeagiza hatua kali kuchukuliwa kwa wale wote watakaobainika kuruhusu ujenzi huo hafifu wa ofisi hiyo nyeti akiwemo Wakala wa Taifa wa Majengo (TBA), aliyekuwa mshauri mkuu wa ujenzi huo. Mchengerwa aliyasema hayo baada ya Kamati hiyo kuwaita viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, ujumbe ulioongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mchengerwa alisema; “Maagizo ya Kamati yanahusu jengo hilo kujengwa chini ya kiwango, kwa hiyo tumeomba tupewe ufafanuzi wa baadhi ya hoja zetu. “Jengo limebainika dhahiri kuwa na nyufa katika baadhi ya maeneo lakini pia kuwepo kwa milango inayohatarisha usalama na hivyo tumeagiza kufanyika kwa ukaguzi wa kina.
“Kwa bahati nzuri leo Waziri (January) ametuhakikishia kuwa tayari wamewasiliana na Wizara ya Fedha Kitengo cha Ukaguzi ili nao wafanye ukaguzi, lakini sisi kama Kamati tumekwenda mbali zaidi kwa kuamua kama Bunge kumuandikia barua CAG ili naye akakague na kutupa jibu ambalo litatuongoza katika kutoa maagizo,” alisema.
Pamoja na hayo, Mchengerwa alisema Kamati hiyo imeagiza mjenzi kutolipwa kiasi cha malipo yaliyosalia akisema taarifa za awali zilionesha kuwa kiasi cha Sh milioni 230 ndizo zilizokuwa zimesalia.
Alisema hata hivyo taarifa za baadaye zilizotolewa na Waziri Januari baada ya Kamati kushangazwa na kubakia kwa kiwango hicho kidogo kuliko ilivyo sheria, zilisema kiasi kilichosalia ni zaidi ya asilimia 10 ya gharama nzima ya mradi. Gharama ya ujenzi wa jengo hilo zilikuwa Sh bilioni nane.

Comments