WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, timu ya Azam FC, jana ilianza vizuri baada ya kuifunga Esprerance ya Tunisia kwa mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Chamazi Complex.
Hata hivyo ushindi huo mwembamba bado haujaihakikisha Azam kusonga mbele na itahitajika ifanye kazi ya ziada ugenini kwa kushinda ama kulazimisha sare na kama itakubali kufungwa iwe kwa tofauti ya bao moja yaani kuanzia mabao 3-2, 4-3 itakuwa imesonga mbele.
Azam FC kama itaitoa Esperance, itatinga hatua ya mchujo kwa ajili ya kusaka nafasi ya kucheza makundi ya michuano hiyo, ambapo itakutana na moja kati ya timu nane zitakazokuwa zimetolewa hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika.
Juzi wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mchezo Afrika uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo wa jana mabao ya Azam FC yalifungwa na Farid Mussa Malik na Ramadhani Singano ‘Messi’ kipindi cha pili baada ya timu hiyo kuwa nyuma kwa bao 1-0 lililofungwa kipindi cha kwanza.
Esperance walipata bao lao dakika ya 33 mfungaji akiwa Haithem Jouini aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Ilheb Mbaark. Nahodha John Bocco alipoteza nafasi zaidi ya mbili kipindi cha kwanza, ikiwemo dakika ya 22 baada ya kupiga nje akiwa amebaki yeye na kipa.
Mshambuliaji mwingine tegemeo wa Azam, Kipre Tchetche alipoteza nafasi dakika ya 36 baada ya kupiga juu akiwa mbele ya goli. Beki wa Azam Muivory Coast, Serge Wawa alishindwa kuendelea na mchezo dakika ya 89 baada ya kuumia misuli na nafasi yake kuchukuliwa na David Mwantika.
Azam; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum/Khamis Mcha ‘Vialli’, Aggrey Morris, Serge Wawa/ David Mwantika, Jean Baptiste Mugiraneza, Kipre Tchetche, Kipre Bolou/Frank Domayo, Ramadhani Singano ‘Messi’, John Bocco na Farid Mussa.

Comments
Post a Comment